Mchezo wa pili kwa Ujerumani na Ghana, timu ambazo zinaunda kundi G pamoja na Ureno na Marekani umemalizika hivi punde huku timu hizo zikitoshana nguvu. Katika mchezo huo ambao ulipigwa katika uwanja wa Castelao ukianza mishale ya saa 10.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki timu ya Ghana imetoa ushindani ambao haukutarajiwa na wengi na kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa hali ambayo iliisababisha Ujerumani kutumia nguvu ya ziada kuweza kulinda heshima.
Tukio ambalo limebaki vichwani na vinywani mwa wapenzi wa soka Duniani ni kufikiwa kwa rekodi ya Mbrazili Ronaldo Delima ambaye ana jumla ya magoli 15 katika michuano ya kombe la Dunia. Mjerumani Miroslav Klose ameifikia rekodi hiyo baada ya kufunga goli la kusawazisha akitokea benchi.
Kwa upande wa Ghana mshambuliaji Asamoah Ghan ameifikia rekodi ya mabao katika michuano hiyo kwa wachezaji wa Afrika baada ya kufunga goli la pili la mchezo ambalo ni la tano kwake katika michuano hiyo. Rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Rogger Millar mchezajia wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon. Ghana kwa sasa wanashikilia nafasi ya 3 katika kundi G wakiwa na point 1 nyuma ya Marekani ambao waliwafunga Ghana katika mchezo wao wa kwanza hivyo wana pointi 3 na Ujerumani wao wana pointi 4 wakiwa wameifunga Ureno katika mchezo wa kwanza na pointi moja ya sare ya leo. Ureno ambao watavaana na Marekani siku ya kesho wao wanaburuza mkia kwa kutokuwa na pointi.
Mchezo uliotangulia ni mchezo kati ya Argentina na Iran ambazo ziko kundi F mchezo ambao ulimalizika kwa Lionel Messi kuifungia Argentina goli pekee katika dakika za nyongeza na kufanya matokeo kuwa 1-0. Mchezo wa kufunga ratiba ya leo ni mchezo kati ya Nigeria na Bosnia.