UMEKUCHA! Unaweza kusema kwa maana nyingine wakati
wasanii kutoka Afrika watakapokuwa pamoja kwenye Ukumbi wa Nokia Theatre
uliopo Los Angeles, Marekani katika sherehe za utoaji tuzo za BET 2014
kesho Juni 29.
Macho na masikio yote yameelekezwa kwa mtu mmoja kutoka Tanzania ambaye ni Nasibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’.
Kupitia
wimbo wa My Number One (Remix), aliomshirikisha staa kutoka pande za
Nigeria, Davido, ndiyo uliompandisha chati za juu mpaka kufikia
kujulikana kimataifa sambamba na kuingizwa katika tuzo mbalimbali za
heshima.
Wapo wanaofurahia mafanikio yake na wengine kuchukia na kuona kama anapendelewa.
Katika makala haya yanachambua safari nzima za tuzo ambazo ameshashiriki na anazoendelea kushiriki kwa sasa;
Awashangaza Watanzania
Aliivunja
rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mwanamuziki Abass Hamis Kinzasa
‘20%’, ya mwaka 2011 ambayo alijinyakulia tuzo tano kwa mpigo
zilizotambulika kama Kilimanjaro Music Awards 2011.
Katika tuzo za
Kilimanjaro za mwaka 2014 zilizofanyika Mlimani City jijini Dar, Diamond
aliondoka shujaa kwa kujizolea tuzo saba kwa mpigo na kuweka rekodi ya
aina yake huku maswali mengi yakibaki midomoni mwa watu na hata wengine
wakidhani amebebwa na hakustahili kupewa tuzo hizo zote.
Atemwa tuzo za MTV MAMA 2014
Mpaka
Diamond anaelekea Afrika Kusini Juni 7 mwaka huu, alionekana kama
msanii anayeongoza kwa kupigiwa kura nyingi na mashabiki akiwa na
asilimia zaidi ya 60. Watanzania wengi walijua ataibuka kidedea.
Wakati
wa ufunguzi wa tuzo hizo alianza kwa kufanya shoo ya nguvu akiwa
sambamba na mwanamuziki kutoka Nigeria, Davido. Walilivaa jukwaa na
wimbo wa My Number One Remix.
Hata wale ambao hawakujua lugha ya
Kiswahili aliyokuwa akiimba Diamond katika wimbo huo walionekana
kumfurahia kwa kucheza naye pamoja.
Kilichokuja kufanyika wakati wa
utoaji wa tuzo hizo, Diamond hakuambulia kitu chochote. Tuzo zilimpita
machoni na kukimbilia kwa wasanii kama Davido, Tiwa Savage, Uhuru pamoja
na Mafikizolo.
Atatoka katika tuzo za BET 2014?
Habari
kila kona ni siku ya kesho Juni 29, katika utoaji tuzo za BET 2014
ambapo Diamond ameingia katika kategori ya Mwanamuziki Bora wa Kimataifa
kutoka Afrika akiwa sambamba na Sarkodie (Ghana), Mafikizolo (Afrika
Kusini), Davido (Nigeria), Toofan (Togo) na Tiwa Savage (Nigeria) ambao
wote kwa pamoja wameshaning’iniza kwapani tuzo za MTV Afrika 2014 na za
BET 2012 kasoro Diamond kutoka Tanzania.
Abaniwa kupafomu
Swali gumu la kujiuliza ni jinsi mpangilio mzima uliopangwa na waandaaji wa tuzo za BET 2014 zitakazofanyika kesho.
Wakati
wale waandaaji wa MTV Afrika 2014 walimpa Diamond nafasi ya kupafomu
wimbo wake kwa kushirikiana na Davido, mambo yamekuwa tofauti kwa BET
2014.
Wamewakusanya wasanii wengi kutoka Nigeria mbaya zaidi ni wale
wanaoshirikiana naye katika kugombea tuzo hizo ambapo kesho watapanda
jukwaani kwa pamoja na kuimba wimbo maalum unaohusu Afrika.
Wasanii hao ni pamoja na Sarkodie kutoka Ghana, Mafikizolo kutoka Afrika Kusini, Tiwa Savage na Davido wote kutoka Nigeria.
Abakiza tuzo mbili tu
Bado
anayo nafasi kubwa ya kusonga mbele na kugombea tuzo mbalimbali za
kimataifa hata kama katika tuzo za BET atazikosa kesho. Mpaka sasa
amebakiza tuzo mbili ambazo ni AFRIMMA 2014 na zile za KORA Africa 2014.