Msanii wa Hip Hop,Bongo Chid Benz (29), amekiri mashtaka matatu yanayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ya kukutwa na dawa za kulevya, kifuu cha nazi na kijiko vinavyotumika kuvutia ama kunusa dawa hizo.
Chid Benz alikiri hivyo juzi Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema baada ya kuomba asomewe tena mashtaka yake. Aliomba hivyo muda mfupi baada ya kesi yake kutajwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Diana Lukendo aliyesema upelelezi haujakamilika hivyo kuomba ipangiwe tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo, Chid Benz alinyoosha mkono na kuiomba mahakama imsomee tena mashtaka yanayomkabili, akasomewa na kukiri kuwa Oktoba 24,2014 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere alikamatwa na gramu 0.85 za Heroin Hydrochloride zenye thamani ya Sh38,638.
Alikiri pia alikutwa na gramu 1.72 za bangi zenye thamani ya Sh1720 na vifaa vinavyounganishwa na matumizi ya kuvuta ama kunusa dawa hizo.
Baada ya kukiri mashtaka hayo yote matatu, Wakili wa Serikali, Lukendo aliiomba mahakama kutoa ahirisho fupi ili waweze kujiandaa na kumsomea maelezo ya makosa yanayomkabili. Hakimu Lema alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hadi Februari 23, 2015.
Awali kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Chid Benz aliposomewa mashtaka hayo aliyakana yote.
CHANZO ;;CloudsFM