Katika jitihada za kuongeza upatikanaji na matumizi ya simu janja ili kuziba pengo la kidijitali nchini, makampuni ya Vodacom Tanzania PLC na Benki ya CRDB wamezindua mpango wa kuwezesha Wateja wao kumiliki simujanja zenye ubora kwa gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo wa kukopesha simu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alieleza kuwa kampuni hiyo ya simu inatekeleza mipango mbalimbali ya kupunguza gharama za vifaa vya mawasiliano ili kuwawezesha wateja wake kuhama kutoka kwenye matumizi ya mtandao wa 2G na kumiliki simu zenye uwezo wa 4G na kutumia fursa hiyo ili kunufaika na faida kemkem zinazopatikana kupitia mtandao huo.
“Tukiwa ni mdau na mshirika mkubwa wa sekta ya mawasiliano na teknolojia, Vodacom tunajivunia kuzindua mpango huu na Benki ya CRDB ambayo ni taasisi kubwa ya fedha nchini. Ushirikiano wetu unalenga kuwawezesha wateja kutoka pande zote mbili kupata aina mbalimbali za simujanja kwa bei nafuu na mpango wa malipo kwa awamu kwa kipindi fulani. Ili kujua kama amekidhi vigezo, mteja atatakiwa kupiga *150*00*44# nbaada ya hapo atafanya malipo ya awali na kupewa simujanja. Mkopo huu unaweza kulipwa kwa siku, kwa wiki au kwa mwezi kwa kipindi cha hadi miezi 12 kupitia M-Pesa,” alifafanua bwana Besiimire.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema, “ushirikiano huu baina yetu na Vodacom ni fursa nzuri kwa Watanzania kupata huduma za kifedha na mawasiliano kwa gharama nafuu. Kwa hiyo kama wadau muhimu tunapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha wananchi wake wanafaidika na ukuaji na maendeleo katika sekta hizi.”
Bwana Nsekela aliongeza kuwa, “Kwa mtandao wetu ulioenea nchi nzima, CRDB tumekuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya Watanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha. Hivyo basi, kwa kushirikiana na Vodacom, tutaweza kutoa mchango wetu ili kuongeza matumizi ya simujanja nchini.”
Licha ya juhudi za mamlaka nchini kusogeza huduma za mawasiliano, wananchi wengi bado wanatumia huduma za mtandao wa 2G. Hii inapunguza upatikanaji wa fursa zilizopo mtandaoni pamoja na kufurahia na kunufaika na intaneti yenye kasi zaidi kutoka Vodacom pamoja na bidhaa nyingine za kidijitali.
Matumizi ya simujanja na intaneti yana faida kwa jamii kama vile kukuza ukuaji wa kiuchumi kwa kuwezesha ujasiriamali wa kidijitali na kuchochea uvumbuzi, utafutaji masoko mitandaoni pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi wanaoamua kujiajili kupitia dijitali.
Vodacom Tanzania imekuwa ikishirikiana na watengenezaji mbalimbali wa simu za mkononi na taasisi za kifedha ili kuwezesha Watanzania kumiliki simu kupitia mikopo nafuu na mipango rafiki ya malipo kwa mteja.
Mwezi August 2020, Vodacom ilizindua programu ambayo inawaruhusu wateja wake kumiliki simujanja kupitia mkopo unaolipwa kwa awamu, huku kianzio kikiwa ni Shilingi 20,000 za Kitanzania kwa muda wa miezi 12.
Bwana Nsekela alimalizia kwamba anaamini kuwa taasisi hizo mbili zina huduma mbalimbali za kibunifu ambazo zitawanufaisha na kuboresha maisha ya wateja wao. Pia alitoa wito kwa Watanzania wanaotumia simu za kawaida na wanataka zenye ubora zaidi kufika katika maduka ya Vodacom na kupata simujanja kwa bei nafuu ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali duniani.
#KonceptTvUpdates