NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imezindua akaunti maalum ya kidijitali iitwayo ‘NMB Niwekee,’ inayolenga kuleta ukombozi wa maisha ya baadaye ya watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira, ambayo inajumuisha faida kedekede ikiwemo Bima ya Maisha yenye fidia hadi ya Sh. Milioni 50.
NMB Niwekee ambayo ni fursa na wepesi wa kuniwekea kifuta jasho cha baadaye, ni akaunti maalum kwa wajasiriamali wadogo na WA kati, watoa huduma wa Sekta ya Usafirishaji kwa Pikipiki ‘bodaboda,’ mama na baba lishe, pamoja na hata waajiriwa wanaopenda kujiongezea vyanzo vya akiba ya uzee iliyo nje ya mifumo rasmi.
Uzinduzi wa NMB Jiwekee uliowakutanisha pamoja ‘Chama la Watunza Pesa,’ umefanyika jijini Dar es Salaam Jumatatu Mei 13, ikizinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi, mwenyeji wa hafla akiwa Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi.
Akizingumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwa mfumo wa kipindi cha runinga kilichoongozwa na Mtangazaji Millard Ayo, Waziri Ndejembi alisema ya kwamba, NMB Jiwekee inayoambatana na faida lukuki kwa wajasiriamali na kada zingine, ni mwendelezo wa juhudi za wazi za taasisi hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali kuyawezesha makundi maalum ya kijamii.
“NMB Jiwekee ni huduma chanya na rafiki kwa watu walio katika mifumo ya ajira isiyo rasmi na wale wenye ajira rasmi wanaotaka kuongeza vyanzo vya akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, ambayo Serikali tunaamini kwamba imekuja kwa wakati sahihi.
“Serikali kila uchao inapambana kuimarisha mahusiano na taasisi za fedha (mabenki) katika kusaidia kutanua WiGo wa Watanzania waliounganishwa kwenye Huduma Jumuishi za Kifedha, na kwa jambo hili taasisi zingine zinapaswa kufuata nyayo za NMB kwa kuanzisha huduma Bora na rahisi, nafuu na salama kama hizi.
“NMB ijikite katika kutoa elimu kwa Watanzania juu ya umuhimu wa huduma hii mpya, lakini pia taasisi zingine ambazo najua zitafuata nyayo hizi za vinara wa huduma za fedha nchini, nazo zitoe elimu ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia mifumo ya kitaasisi katika utunzaji wa akiba.
“Serikali haiwezi ‘ku-cover’ kila kitu ndio maana tunasisitiza nguvu za wadau hususani taasisi za fedha katika kuwaunganisha Watanzania na Huduma Jumuishi za Fedha.
“Zaidi niwapongeze NMB kwa kuwapa uhuru watumiaji wa NMB Jiwekee wa kuchagua asilimia za kujitunzia kutokana na matumizi ya fedha zilizo kwenye akaunti zao,” alisema Waziri Ndejembi.
Akizungumzia jitihada za Serikali katika kupunguza umaskini kwa wananchi, Waziri Ndejembi alisema kipaumbele cha awali kilikuwa ni kurasmisha makundi na sekta zisizo rasmi, ili kuwawezesha wahusika kutambulika, kukopesheka na kuwa sehemu wa wachangiaji wa Pato la Taifa.
“Mfano wa juhudi hizo ni ile Programu ya Kujenga Kesho Iliyo Bora kwa Vijana na Wanawake (BBT), ambako tuna BBT Kilimo, BBT Ufugaji na Uvuvi, zote hizo ni jitihada za kupunguza umaskini kwa Watanzania, pamoja na ule Mpango wa ‘Four Four Two’ unaojumuisha asilimia nne ya fedha za mikopo kwa akina mama, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa wenye ulemavu,” alisema Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake, Filbert Mponzi, akijibu maswali ya Millard Ayo aliyetangazwa kuwa Msemaji wa ‘Chama la Watunza Pesa,’ alisema NMB Jiwekee ni zao la tafakuri za kina zilizofanywa na benki hiyo katika kufanya mapinduzi ya ukombozi wa maisha ya watu wasio na ajira rasmi.
“NMB Jiwekee ni zao la maswali juu ya watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira na wale ambao hawajaajiriwa kabisa, juu ya utunzaji akiba zao kwa maisha ya baadaye, tunajua ipo mifumo rasmi ya akiba kwa waajiriwa kama Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Tukajiridhisha kuwa NSSF ni kwa waajiriwa, inakuwaje kwa watu wasio na ajira ama wale ambao hawana ajira rasmi, ndipo likaja wazo lililozaa NMB Jiwekee ambayo ni kwa kila mmoja miongoni mwa wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo, bodaboda, mama na baba lishe na makundi mengine kwenye Sekta zisizo rasmi.
“Uwekaji akiba hutokana na pato la mfunguaji wa NMB Jiwekee linalopitia katika benki yetu, ama waweza kuweka kwa kupitia miamala ya simu za mkononi kutunza pesa kidijitali na kunufaika na faida nyingi zilizomo, ikiwemo akiba ya baadaye, riba ya asilimia tano ya akiba kwa mwaka na bima ya maisha.
“Bima hii itakuwa na fidia mara mbili ya akiba yako uliyojiwekea katika NMB Jiwekee, ama hadi shilingi Milioni 50 ya fidia upatapo ulemavu wa kudumu utakaokufanya ushindwe kuendelea kujiwekea akiba. Kianzio kwa njia ya akaunti kinaanzia asilimia moja hadi 100 ya pesa zako zinazopitia NMB,” alibainisha Mponzi mbele ya waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo.
Mwishooo