Na Mwandishi Wetu
Benki ya NMB imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Comoro ikiwa ni dhamira ya benki hiyo kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Uhuru wa nchi ya Comoros iliyoandaliwa na Ubalozi wa Comoro nchini Tanzania kwa udhamini wa Benki ya NMB, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Rahma Mwapachu alisema benki hiyo inathamini maadili na urithi wa nchi hiyo.
“Benki ya NMB ina uhusiano mzuri na Ubalozi wa Comoro. Tuna matumaini kuwa uhusiano huu utaimarika zaidi na utafungua fursa nyingine,” Rahma alisema.
Bi. Mwapachu alisema benki imejidhatiti kuendelea kutoa masuluhisho ya biashara ya kipekee na yenye ubunifu ili kuhakikisha uongezaji wa thamani kwa wateja wake.
“Ubalozi wa Comoro umenufaika kutokana na suluhu zetu zilizoundwa mahususi ikiwa ni pamoja na malipo ya visa ya kidijitali, akaunti maalum za kitaasisi na masuluhisho ya kifedha yaliyoundwa mahususi,” aliongeza.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga wakati wa hafla hiyo alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Comoro ili kuzidisha uhusiano wa karibu kwa manufaa ya taifa.
Alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Comoro kimeongezeka kutoka dola zakimerikani milioni 6.75 mwaka 2001 hadi kufikia dola milioni 54 mwaka 2023.
“Hii imeifanya Tanzania kuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Comoro,” alisema