Katibu Tawala wa mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari amewataka watoa huduma za Afya katika mkoa huo kujaza kwa usahihi na kufuatilia fomu za madai fedha ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili fedha hizo zitumike kuboresha huduma za Afya.
Bi. Omari ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku mbili ya timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na mkurugenzi Dkt. Rashid Mfaume ambapo amesisitiza wataalamu wa Afya kufuatilia kikamilifu ili fedha hizo zipatikane.
“Mnasema hela zimekusanywa kwenye NHIF lakini ‘claim’ hazipo na hazieleweki ziko hovyo hovyo sasa sijui nani hampendi mwenzie kwasababu hela hizi zikikusanywa zinatumika na idara husika au hampendi kulipwa sitahiki zenu ipasavyo au mishahara ni mikubwa inatosha na kwa hili watumishi wa Afya hamsomeki vizuri”
Katika hatua nyingine Bi. Judica Omari ameshangazwa na matumizi hafifu ya asilimia 63 ya ‘User Fee’ (malipo ya papo kwa papo) wakati vituo vinahitaji dawa,vifaa tiba na sitahiki za watoa huduma katika mkoa wa Njombe.
Kwa upende wake Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ameelekeza maeneo ya kutolea Huduma za Afya kuajiri watumishi kwaajili ya ufuaji badala ya kuwapangia zamu watoa huduma. “tumeenda kituo cha Afya Lyamkena tumekuta watumishi wenyewe ndio wanafua mashuka na zingine zimechanganyika na damu za wagojwa na hilo sio sawa kwahiyo ni marufuku watumishi wetu wa Afya kufanya kazi hizo wakati tunawategemea kutoa huduma” Bi. Judica ameipongeza timu hiyo kwa kufanya usimamizi shirikishi na ufuatiliaji wa utolewaji wa huduma za Afya ambao umekuwa chachu na elimu kwa watumishi wa sekta ya Afya.
Cc:Tamisemi