Na Mwandishi Wetu;
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishauri Denmark kuongeza masuala ya ushirikiano katika sekta za nishati, maendeleo ya sekta ya fedha na kukuza uwekezaji katika mpango wao mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoandaliwa na nchi hiyo.
Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo wakati akimuaga Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, katika Ofisi za Hazina Ndogo, Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Dkt. Nchemba alimshukuru Balozi Dissing-Spandet kwa kufanikisha kusitishwa kwa uamuzi uliotaka kuchukuliwa na nchi yake wa kufunga ubalozi wake hapa nchini na kwa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Denmark.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa mchango wa Denmark katika maendeleo ya nchi umekuwa mkubwa katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR, sekta ya afya, utawala bora, kukuza ajira, demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu, miradi ambayo alisema inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umasikini wa wananchi.
Alimwomba Balozi huyo kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika kuhamasisha kampuni za Denmark kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea na miradi ya nishati kwa njia ya upepo.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, alisema kuwa anajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini ambapo ameshuhudia nchi ikipiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii.
Aliahidi kuwa ataendelea kuwa balozi mzuri wa Tanzania ili kuvutia uwekezaji na kwamba kampuni nyingi za nchi yake zimeonesha nia ya kuwekeza hapa nchini.
Alisema kuwa alama kubwa anayoiacha ni pamoja na kuishawishi nchi yake kuachana na mpango wa kufunga shghuli za kibalozi hapa nchini na kwamba hatua hiyo itaiwezesha Denmark kujipanga upya na kuja na mpango mkubwa wa kushirikiana na Serikali katika kukuza maendeleo ya nchi.