Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 08 Julai, 2024.
Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo, Dkt. Kijaji alionesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo huku akimtaka Mkandarasi Kampuni ya SUMA JKT kuongeza kasi ya ujenzi ili likamilike kwa wakati na hatimaye lianze kutumika.
Dkt. Kijaji aliishukuru Kampuni ya SUMA JKT ambayo imepewa kazi ya kutekeleza mradi huo kwa hatua iliyopiga pamoja na kamati iliyoteuliwa kuusimamia ujenzi huo. “Mradi huu tunatakiwa tuukamilishe mwezi Novemba mwaka huu lakini ikiwezekana hata ukamilike haraka zaidi kwani hakuna kipingamizi cha kufikia malengo hayo kwani fedha zipo na zinaendelea kutolewa na Serikali kwa Wizara zote” alisema Kijaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alimshukuru Waziri Kijaji kwa ziara ya kukagua jengo hilo na kusema litaongeza kasi na morali kwa Mkandarasi na Mshauri Elekezi wa mradi huo.
“Malengo ya Serikali ni kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili uweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais…Rai yangu ni kuwasihi kuikamilika kazi hii ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba uliopo,” alisema Mhe. Khamis.
Nae Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi alisema jengo hilo limejengwa katika mfumo wa kisasa wenye mazingira Rafiki na wezeshi kwa ajili ya kutoa huduma kwa viongozi,
watumishi na wananchi.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya usimamizi wa Jengo hilo ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Paulo Laizer alisema kazi mbalimbali zinaendelea kutekelezwa kulingana na mpango kazi uliowekwa na ofisi. Laizer alisema Menejimenti ya Ofisi imejipanga kuhakikisha kuwa mkandarasi wa ujenzi wa jengo pamoja na Msimamizi Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wanaendelea kusimamiwa kwa karibu zaidi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
“Tumepokea maelekezo yako Mhe. Waziri na tumejipanga kuyatekeleza ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na watumishi wote ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wanahamia kwa wakati katika jengo hili” alisema Laizer.
Ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ni ya kwanza kwa Dkt. Kijaji tangu alipoteuliwa na kuapishwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akitokea Wizara ya Viwanda na Biashara.