Golikipa wa klabu ya Gremio Anapolis, Ramon Souza amepata jeraha kwenye paja la mguu wa kushoto baada ya kupigwa risasi na afisa wa Polisi wakati wa mzozo kati ya timu yake na Centro Oeste zote za Brazil, mara baada ya mchezo wao kumalizika.
Kipande cha video kilichochukuliwa Uwanjani hapo na kusambazwa kwenye mitandao ya kijami, ilionyesha tukio hilo lililosababishwa na mvutano wa timu hizo baada ya Gremio Anapolis kupoteza kwa mabao 2-1.
Viongozi na wachezaji walikuwa wakizozana kabla ya askari huyo kuonekana akifyatua risasi ya mpira na kumpata Souza iliyotoboa paja lake na kumsababishia maumivu kabla ya kuwahishwa hospitali kwa gari la wagonjwa.
“Anapolis imesikitishwa na tukio lililotokea katika Uwanja wa Jonas Duarte, Jumatano na baada ya mchezo dhidi ya Centro Oeste, kipa wetu Ramon Souza alipigwa risasi ya kipira na Polisi, kitendo hiki ni sawa na uhalifu tena kimefanywa na mtu ambaye alitakiwa kuhakikisha usalama wa watu waliokuwa uwanjani.”
“Siku hii ya tukio (Julai 10), imekuwa siku mbaya kuwahi kutokea kwetu na wachezaji wetu kamwe hawatoisahau. Tumedhamiri kufuata hatua stahiki kuhakikisha mhusika anachukuliwa hatua kutokana na kitendo chake hiki.” Imesema taarifa ya klabu hiyo kwenye mitandao ya kijamii.