Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Mtume Boniface Mwamposa amesema kuna makundi mawili yanayomfuatilia, wapo wanaomkubali kuwa ni mpaka mafuta na wengine wanatarajia akosee neno, ili wamuharibie kazi.
Akihubiri wakati wa ibada kanisani kwake eneo la Kawe amesema watu wanaomfuatilia wapo kwa ajili ya kusikiliza waone amekosea neno ili walipindue, walitumie kuharibu kazi ya Mungu anayoifanya.
“Soma maandiko acha kutafsiri sawasawa na wapinzani wa kazi ya Mungu, nazungumza na wanaonifuatilia si ninyi,” amesema Mwamposa.
Amesema kazi anayoifanya si ya Mwamposa ni kazi ya Mungu aliye hai, hivyo wanatakiwa kufuata maandiko ya kitabu cha Biblia.
“Nataka nikupe siri, acha kujali watu wanaongea nini endelea na majukumu yako ya kazi, mipango yako na wao watakutafuta tu,” amesema Mwamposa.
Amesema Biblia inasema: “Huyu ndiye akatuma mtu naye akamleta kwao naye alikuwa mwekundu mwenye macho mazuri na umbo lake la kumpendeza bwana akasema ondoka mtie mafuta maana huyu ndiye, ndipo Samwel akatoa pembe yenye mafuta akamtia mafuta kati ya ndugu zake na roho ya bwana ikamlilia Daudi kwa nguvu.”
Mwamposa amesema waelewe kanuni iliyopo kabla ya kumwagiwa mafuta, Mungu alikuwa mbali, lakini alipomwagiwa mafuta tayari roho ya kifalme ikashuka juu ya Daudi akaanza kufanya kazi, kutembea na kuwa na ufahamu.
“Someni Biblia mtaelewa mambo ya Mungu yapo wazi utachukua mafuta na maji ya upako utayaombea na kuachilia kwa watu, kisha wanapewa maelekezo aliyopewa na Mungu na si kuchanganya na kitu kingine,” amesema.
“Kuna mambo lazima uyaelewe watu wa giza wanachukua kitu hiki na kile wanachanganya, lakini hawa wana mambo mengi ya uharibifu. Ukija kwa Mungu kinachofanya kazi ni upako, ni nguvu ya Mungu na inafuatana na mafuta, kwa mafuta kiongozi wa kiroho amekwambia ufanye nini,” amesema na kuongeza;
“Ukitaka ufaulu kaa chini ujifunze usililojua kwako ni usiku wa giza, sikiliza ujifunze mbona Mtume Buldoza yupo kwenye runinga na redio, wapo watu wanasema hawataki kumsikiliza wamekosa hekima wanatakiwa wasibishane na kitu ambacho hawajakisikiliza kimaandiko halafu wajue cha kufanya.
Amesema wapo baadhi ya Watanzania wamemkataa, lakini watu kutoka mataifa mbalimbali kama Ubelgiji, Uganda, na Uholanzi wamekuja nchini kupokea uponyaji na wanamuamini.
Chanzo : Mtandao