Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Simon Patrick amesema Club imegundua Walalamikaji Juma Ally na Geofrey Mwaipopo waliofungua kesi wakitaka Rais wa Club hiyo Eng. Hersi Said na Viongozi wengine waachie ngazi, walighushi sahihi ya Club, sahihi ya Mama Fatma Karume na sahihi ya Jabir Katundu ili kushinikiza Mahakama iwape ushindi na iridhie wapewe Timu na mali zote za Club waendeshe wao.
Akiongea leo July 17,2024 Jijini Dar es salaam, Simon amesemaa “Watu wawili Juma Ally na Geofrey Mwaipopo waliojiita Wanachama wa Yanga November 2022 walifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwenye kesi hiyo msingi wa madai yao walikuwa wanadai hawalitambui Baraza la Wadhamini la Yanga na kutokana na kutoitambua Katiba ya 2010 ambayo haijasajiliwa na RITA wanadai Wanachama wote sio halali hivyo Viongozi wote na Wanachama wote ambao waliingia kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 2010 ni batili wakimaanisha Rais wa Club Eng. Hersi, Makamu wake na Viongozi wote uanachama wao ni batili hivi walikuwa wanaiomba Mahakama ituondoe katika Uongozi, na la tatu walikuwa wanataka kazi zote zilizofanywa na Viongozi hawa zitambuliwe kama batili na waletewe mapato na matumizi yote kwao”
“Kesi ilianza kusikilizwa Mlalamikiwa namba moja ikiwa ni Club ya Yanga, Mama Fatma Karume Mlalamikiwa namba mbili na Mzee Jabir Katundu Mlalamikiwa namba 3, ambapo Abeid Mohamed Abeid aliwasilisha ushahidi au utetezi ambao ulisainiwa na Club, Mama Fatma na Jabir Katundu akidai wote wamemteua kuwawakilisha katika mwenendo wa kesi hiyo, na Abeid alikuwa anakubali kila kitu kinacholalamikiwa akidai anawawakilisha wengine na ikapelekea Mahakama kuwapa ushindi Walalamikaji August 08,2023”
“Mwezi May 2024 Walalamikaji hao walipeleka maombi ya kukaza hukumu mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba Mahakama iwasaidie kulitoa na kulifuta Baraza zima la Wadhamani wa Club na kuutoa Uongozi wote wa Club na kutaka wakabidhiwe Timu na asset zote za Club waendeshe wao, Eng Hersi akaelekeza tufuatilie tukabaini wameghushi sahihi na pia Walalamikaji hao sio Wanachama wa Yanga”