Mwanamke ambaye hakuweza kutambulika jina lake, amenusurika kifo baada ya kutuhumiwa kuiba mtoto wa miaka 5, ambaye alikuwa akicheza nje ya nyumba yao, eneo la Mtaa wa misheni Makuka Kijichi Darajani.
Polisi eneo la Kijichi wamemuokoa mwanamke huyo, aliyekuwa amezungukwa na raia wenye hasira ,ambao walishaanza kujichukulia sheria mkononi, huku wengine wakiwa kwenye taharuki kwa kilichojitokeza.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam, yakionesha vitendo vya utekaji Watoto kushamiri hali ambayo imekuwa ikiogofya huko mtaani.
Julai 19, 2024, taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, DCP, David Misime, ilieleza kuwatoa hofu wananchi juu ya wimbi la baadhi ya watu wenye nia ovu ,wanaotunga taarifa za uongo kuwa eneo fulani watoto wa shule fulani wamechinjwa kisha kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambapo aliwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida wakati, wakiwasaka watu hao wanaovunja sheria kwa makusudi na kuleta hofu na taharuki kwa jamii, ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Taarifa ya DCP Misime ilieleza kuwa ,taarifa hizo zimekuwa zikileta taharuki, usumbufu na mshtuko kwa wazazi, walezi na watoto, na kubainisha kuwa tabia hiyo pamoja na kwamba ni kosa la jinai, lakini ni tabia ya kulaani na kukemewa kwa nguvu kubwa na kila mmoja mwenye kuchukia tabia kama hizi za watu wachache.
Chanzo : ITV