Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Uhamiaji Nchini kutembelea na kufanya ukaguzi kwenye vituo vya uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la Wapiga kura ili kuwabaini Watu wasio Watanzania wanaotaka kujipenyeza kuandikishwa kwenye daftari hilo.
Waziri Mkuu amesema hayo katika uzinduzi wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika katika uwanja wa Kawawa Manispaa ya Kigoma Ujiji July 20,2024 ambapo amesema kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa katika daftari hilo.
Amesema Mwananchi ndiye Mtu wa kwanza kutambua nani ni Mtanzania na nani sio Mtanzania katika maeneo wanaoishi hivyo kuwe na ushirikiano baina yao ili kutambua wasio na sifa ya utanzania na kuhakikisha kuwa hawajiandikishi katika daftari hilo na kufanya zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Watanzania lazima tuwe Wazalendo, upigaji kura ni kwa sisi Watanzania, tunachagua Viongozi watakaoliongoza Taifa la Tanzania, tunachagua Viongozi ambao watakuja kuwa Viongozi wa mitaa yetu na vitongoji vyetu, kwanini kuruhusu Mtu wa nje aje atupigie kura? atatuamlia ambavyo sisi hatutaki, kwahiyo tusiruhusu Mtu yoyote kutoka nje ajiandikishe katika daftari la mpiga kura”