Haji Manara akizungumza na wanahabari, Serena Hotel, jijini Dar es Salaam amesema adhabu yake ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka miwili (2) iliyokuwa imetolewa na shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) imemalizika rasmi, Jumapili Julai 21, 2024 hivyo kwa sasa yuko huru kuendelea na majukumu yake kama mwajiriwa wa Yanga SC kama Msemaji wa klabu hiyo.
Manara amemaliza adhabu yake aliyofungiwa kujihusisha na mpira ndani na nje ya nchi. Manara alifungiwa miaka miwili pamoja na faini ya milioni 10 baada ya kukutwa na hatia ya kumkosea nidhamu Rais wa TFF, Wallace Karia.
Manara aliyekuwa ameambatana na familia yake kwenye kikao hicho amesema sambamba na kutumikia ‘kifungo cha soka’ cha miaka miwili pia amelipa faini ya shilingi milioni 10 za Tanzania iliyokuwa imeambatanishwa kama sehemu ya adhabu yake.
Alipoulizwa ni kwa jinsi gani atakwenda kufanya kazi klabuni hapo ikizingatiwa kuwa majukumu anayokusudia kwenda kufanya kwa sasa yanafanywa na AllyKamwe (Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga SC) Manara amejibu kuwa yeye ndiye msemaji wa Yanga SC na kwamba kabla hajafungiwa amefanya kazi kwa takribani mwaka mmoja (1) na Hassan Bumbuli (Aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC) bila kuingiliana kwenye majukumu kwa kuwa kila mtu alifanya majukumu yake, hivyo ni matumaini yake kuwa hata kwa waliopo sasa itakuwa hivyo.
Manara amekanusha madai ya kuwa Ali Kamwe ni ‘Boss’ wake badala yake ameendelea kutoa msisitizo kwa wanahabari na Watanzania kwa ujumla kufahamu kuwa wawili (2) hao kila mmoja anatimiza majukumu yake. “Mimi nafanya kazi na mtu yeyote yule, Ofisa Habari sio Boss wa Idara, narudi Yanga SC kama Msemaji wa klabu na interest yetu ni mpira na sio kwenda kuchukua kazi za watu.
“Niko tayari kuitumikia klabu yangu ya Yanga, niliiacha nikiwa msemaji baada ya kufungiwa na bila shaka Yanga wataniambia unakwenda kuwa nani, tusubiri viongozi, kamati ya utendaji irejee, hilo ni jukumu lao sio langu,” amesema Manara