Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema limefuatilia kwa kina taarifa zilizosambazwa July 22, 2024 kwenye mitandao ya kijamii na kuzua taharuki na hofu kwa Wananchi eneo la Mburahati zinazodai kuwa Watoto wawili wa Shule ya Msingi Brayson iliyopo Mburahati Wilaya ya Ubungo wametekwa na gari aina ya Noah Nyeusi ambayo haikuwa na namba za usajili ambapo Polisi imejiridhisha ni taarifa za uongo na uzushi.
Akiongea Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Muliro Jumanne amesema “Tulifuatilia kwa kina taarifa hizo na kugundua kuwa ni za uongo, uzushi na ni muendelezo wa taarifa ambazo zimekuwa zinazushwa kwa lengo la kuzua taharuki na kutia hofu kwa Wananchi dhidi ya Watoto na Wanafunzi”
“Baadhi ya taarifa zilizowahi kuzushwa ni kama zile za Mbagala, Shule ya Msingi Kisewe zilizodai Wanafunzi kuuwawa, kuchukukiwa figo na kunyofolewa macho ambazo zilithibitika kuwa ni za uongo, Kigamboni taarifa hizo zilidai Watoto wanne wameuwawa na kuwekwa kwenye viroba ambazo pia zilikuwa za uongo na eneo la Kipawa katika Shule ya Sekondari Majani ya Chai taarifa zilidai Wanafunzi watatu kuuawa pia zilibaini kuwa ni uongo na uzushi”
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za kisheria lilimkamata Mtu mmoja kwa tuhuma za kuzusha taarifa za uongo za tukio la Mbagala, pia Jeshi linawatafuta wengine wote wanaonzisha na kusambaza taarifa hizo za uongo na wakikamatwa watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria, tunawataka Wananchi wote kuacha kusambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo na nyingi zimethibitishwa kuwa ni za uongo zenye kuzua taharuki”
“Jeshi la Polisi linawashauri Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Jeshi katika kuhakikisha Watoto wanaendelea na masomo bila hofu”