Shirikisho la soka nchini (TFF) limethibitisha kuwa Haji Manara amemaliza kifungo chake cha miaka miwili na wamepokea pesa Tsh Milioni 10 kutoka kwa Manara kama sehemu ya adhabu yake hivyo na kubainisha kuwa kwa sasa yupo huru kurudi kwenye shughuli mbalimbali za soka
“Manara yuko huru kweli, na hata huo mkutano alioufanya hajakosea kitu kwa kuwa hajafanya kosa lolote kikanuni, adhabu yake ilimalizika” amesema Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.
“Ukiacha kumalizika kwa adhabu yake pia TFF lishapokea malipo ya faini yake ya sh 10 Milioni, malipo hayo aliyafanya wikiendi iliyopita,” ameongeza Ndimbo.
Haya yanajiri saa chache baada ya Manara kutangaza kurejea katika majukumu aliyokuwa anafanya awali baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa kwa miaka miwili iliyotolewa na Kamati ya Maadili ya TFF.
Manara alikumbana na adhabu hiyo kutokana kudaiwa kufanya makosa ya kimaadili alipokwaruzana na Rais wa TFF, Wallace Karia, katika Fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union ya Tanga, uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha mnamo Julai 2, 2022.