Wananchi watakaofanya udanganyifu ili wajiandikishe zaidi ya mara moja wanatenda kosa na wakibainika wanaweza kufungwa jela kifungo kisichopungua miezi sita na kulipa faini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita.
“Ningependa kusisitiza kuhusu suala la kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja, jambo hili ni kosa la kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024,” amesema.
Jaji Mwambegele amefafanua kuwa kifungu hicho kinasema mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa mtu kujiandikisha mara mbili na taarifa zake kusalia kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwa kabla ya kutoa nakala ya mwisho, Tume hulisafisha Daftari kwa kuwaondoa wapiga kura waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
“Mara baada ya uandikishwaji wa wapiga kura kukamilishwa, taarifa zote huingizwa kwenye mfumo wa AFIS (Automated Finger Print Identification System) ambao huwaonesha wote waliojiandikisha kwenye Daftari zaidi ya mara moja. Wapiga kura wa aina hii hufutwa moja kwa moja kwenye vituo vyote na kuwabakisha kwenye kituo alichojiandisha mara ya mwisho,” amesema.
Ameongeza kuwa orodha ya waliojiandikisha zaidi ya mara moja hupelekwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria na kwamba Tume imefanya hivyo katika chaguzi za nyuma ambapo katika uandikishaji uliofanyika mwaka 2015, Tume ilibaini jumla ya wapiga kura 52,078 waliojiandikisha zaidi ya mara moja ambapo orodha yao ilikabidhiwa kwa Jeshi la Polisi tarehe 27 Agosti, 2015 kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Katika uboreshaji wa Daftari wa mwaka 2020, Tume ilibaini majina ya watu 42,301 ambao walijiandikisha zaidi ya mara moja na orodha hiyo ilikabidhiwa kwa vyombo vinavyohusika na makosa ya kijinai,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa uchakataji wa Daftari, Tume huchapisha na kuweka wazi Daftari hilo chini ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya mwaka 2024 ambapo wananchi hulikagua.
“Baada ya kukamilika kwa uchapishaji wa mwisho wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vyama vya siasa hupewa nakala tepe (soft copy), haijawahi kutokea jina likajitokeza zaidi ya mara moja. Hivyo, hakuna uwezekano wa mtu kuandikishwa zaidi ya mara moja na kuweza kutumia nafasi hiyo kuwa kwenye vituo zaidi ya kimoja siku ya kupiga kura,” amesema Jaji Mwambegele.