Waziri wa nchi Ofisi ya Rais-Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025-2050 unashirikisha wananchi kama njia sahihi ya kujenga mwafaka wa kitaifa kwa kuwa na makubaliano ya pamoja ya kule taifa linapotakiwa kufika.
Prof. Kitila ametoa kauli hiyo mapema siku ya Jumamosi tarehe 27 Julai 2024 akifungua Kongamano la Pili la Kikanda Kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025-2050 linalofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyetaka wananchi kushirikishwa kwenye uandaaji wa dira ya maendeleo.
“Lengo hapa ni kwamba tunataka tufike mahali tukubaliane kama Taifa juu ya mambo ya msingi tunayoyataka. Kwa maneno mengine mchakato wa kuandaa dira unatarajiwa kutuunganisha na kutufanya tukubaliane kuhusu safari tuendako na kama ni kutofautiana iwe ni juu ya namna na njia za usafiri za kutufikisha katika safari yetu.” ameongeza Prof. Kitila.
Aidha Waziri Kitila amesema dira hiyo ya maendeleo ni dira ya wananchi na si ya serikali na hivyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliona ni muhimu kupata maoni, ushauri na mapendekezo ya wananchi ili kupata dira itakayokuwa shirikishi na jumuishi na yenye kuzingatia na kutekeleza mahitaji na changamoto za wananchi wa Tanzania.