Kama mdhamini mkuu wa mbio za Kilomita 21 katika NBC Dodoma Marathon 2024, kampuni ya mawasiliano na teknolojia Vodacom Tanzania ikiwakilihwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Philip Besiimire ilishiriki katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa mbio hizo sambamba na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw. Theobald Sabi na viongozi wengine mbali mbali.
Akizungumza kabla ya utoaji wa zawadi hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania alieleza kuhusu msukumo wa kampuni hiyo ya mawasiliano kuunga mkono mbio hizo kwani zinaenda sambamba na jitihada zao katika eneo la afya ya uzazi ambapo kwa zaidi ya miongo miwili, Vodacom kupitia Vodacom Foundation imekuwa ikijitolea kuimarisha eneo hilo.
“Tumewekeza zaidi ya dola milioni 20 za Kimarekani katika miradi ya kijamii, ambapo zaidi ya asilimia 65% imeelekezwa kwenye afya ya uzazi. Programu maarufu ya m-mama pekee imechangia kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 38% na kuwezesha usafiri wa dharura kwa wanawake zaidi ya 100,000 kwenda hospitalini, hivyo kuokoa maisha ya mama na mtoto. Vile vile, tumeunga mkono na kuboresha maisha ya wanawake zaidi ya 20,000 kupitia msaada wetu kwa wanawake wanaopitia upasuaji wa kurekebisha na ukarabati kwa wale wanaosumbuliwa na fistula ya uzazi. Tumedhamini mbio hizi ili kusaidia ufadhili wa masomo na mafunzo ya wakunga na kambi za matibabu (medical camps) ya saratani ya shingo ya kizazi.” alisema Bw. Besiimire.
Mbali na zawadi za fedha taslimu zilizotolewa na benki ya NBC, Vodacom pia iliwapatia zawadi mbali mbali washindi wa mbio hizo.