Idara ya Uhamiaji mkoani Mbeya imemkamata Dismas Nziku kwa tuhuma za kutengeneza vyeti bandia vya kuzaliwa vinavyofanana na vile vinavyotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), pamoja na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mrakibu wa Idara ya Uhamiaji mkoani humo, Gerhard Mardai amesema kijana huyo aliyekamatwa Julai 29,2024 katika eneo la Sokomatola jijini humo, alikutwa pia akiwa na mihuri bandia ya taasisi mbalimbali za umma, leseni ya kufungisha ndoa pamoja na fomu za kuombea mikopo ya elimu ya juu.
Mardai amesema Nziku atafikishwa mahakamani mara baada ya shauri lake kupelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.