Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kukagua jumla ya miradi 14 ya kimaendeleo inayohushisha sekta mbalimbali ambayo imetokana na uwekezaji wa serikali ya awamu ya sita Mkoani Morogoro katika ziara yake ya kikazi itakayodumu kwa muda wa siku sita mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2024 Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima ameeleza kuwa ziara hiyo itaanza Agosti 02 hadi 07, 2024 ikiwa na lengo la kutangaza fursa za kiuchumi na Uwekezaji ikiwemo fursa za kibiashara pamoja na utalii.
Kati ya miradi ambayo Rais Samia atakagua ni pamoja na kiwanda kipya cha Sukari cha Mkulazi, kufungua Barabara ya Dumila Ludewa na Kilosa na vilevile kukagua miradi iliyopo katika wilaya ya Kilombero.
Kwa upande wao wakazi wa Mkoa wa Morogoro wamefurahishwa na ujio huo wa Rais kwani ujio wake utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo changamoto ya Maji na Miundombinu ya Barabara.