Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imezitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza juhudi za kujikinga na kujilinda na ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi wake.
Tahadhari hiyo inafuatia ripoti ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kuzitangaza Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Burundi imethibitisha kuwa na wagonjwa watatu wa Mpox kwenye miji ya Bunjumbura na Isare huku sampuli za vimelea vya maambukizi kwa wagonjwa hao vikithibitishwa na maabara ya WHO.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa nchi ya tatu kutangaza kuwepo kwa mlipuko wa Mpox nchini humo huku pia Rwanda ikiripotiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa na mlipuko wa Mpox.
Kwa mujibu wa WHO, tangu mwaka 2022, DRC imewahi kuwa na wagonjwa 21,000 na zaidi ya vifo 1,000 vitokanavyo na Mpox huku wengi wa waliogua na kufariki kwa ugonjwa huo wakiwa watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano.
Burundi inapakana na DRC, Rwanda na Tanzania huku DRC ikipakana na nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki: Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini.
CHANZO: Jumuiya ya Afrika Mashariki