Msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2023/24 umefikia tamati na usiku wa tuzo za ligi kuu ya NBCPL umewaheshimu wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika timu zao. Kutoka katika timu mbalimbali, wachezaji hawa wameonyesha ubora wao na kujipatia nafasi katika kikosi bora cha msimu huu. Ifuatayo ni orodha ya wachezaji waliounda kikosi bora cha NBCPL:
Kwa kuanza na golikipa Lay Matampi (Coastal Union), ni mwiba kwa kila safu ya ushambuliaji ya timu pinzani awapo uwajanji, unaweza kusifu uwezo wake na kupongeza kwa mchango wake golini, amekuwa muhimu kwa timu yake, akifanya kazi kubwa katika kudhibiti mashambulizi ya wapinzani.
Safu ya ulinzi kwa maana ya mabeki, ni sehemu ambayo imepambwa na Kouassi Yao (Yanga SC) ambaye mara zote ameonyesha uimara na umakini mkubwa katika safu ya ulinzi na uwezo mkubwa katika kupandisha mashambulizi huku akihusika katika magoli kadhaa. Wakati ukistaajabu hayo kuna Mohamed Hussein (Simba SC), ni beki mwenye uwezo wa kucheza kwa ufanisi katika ulinzi na kushambulia.
Ibrahim Bacca (Yanga SC), mefanya kazi kubwa katika kuhakikisha usalama wa lango la timu yake, akithibiti safu ya ushambuliaji ya timu pinzani. Dickson Job (Yanga SC), licha ya kuwa na umbo na kimo kifupi kiasi, lakini hiyo huenda ikawa ndiyo sababu inayomsukuma kucheza vizuri, ni mchezaji mwenye nguvu na uthabiti mkubwa katika safu ya ulinzi.
Katika safu ya viungo, Feisal Salum (Azam FC), ameonesha ustadi mkubwa katika kusambaza mipira na kusaidia safu ya ushambuliaji. Mudathir Yahaya (Yanga SC), ni kiungo bora mwenye uwezo wa kudhibiti mchezo na kufanya mashambulizi. Kipre Junior (Azam FC), ameonyesha uwezo wa hali ya juu katika safu ya kiungo, akichangia mabao na kutoa pasi za mwisho.
Aziz Ki (Yanga SC), amefanya kazi nzuri katika kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji. Pia, ndio kinara wa upachikaji mabao kwa upande wa Young Africans SC, ni mchezaji anayeimbwa sana katika kurasa, vilabu na vinywa mbalimbali vya watu kutokana na uwezo wake.
Nafasi ya washambuliaji imepambwa na Maxi Nzengeli (Yanga SC), ambaye mara zote ameonesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kusaidia timu yake kupata ushindi. Unaweza ukapata tabu kutafsiri moja kwa moja anacheza namba gani uwanjani kwa maana kila mahali yupo. Kadhalika, Wazir Junior (KMC), ameibuka kama mshambuliaji hatari, akifunga mabao muhimu na kusaidia timu yake.
Hawa ndio wachezaji waliotajwa kuwa bora katika nafasi zao kutokana na mchango wao mkubwa katika msimu wa 2023/24.
#KonceptTvUpdates