Leo, tarehe 5 Agosti 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepiga hatua mpya katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutangaza ongezeko la bei ya mpunga kutoka shilingi 570 hadi shilingi 900 kwa kilo. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya 6 za kuwanufaisha wakulima na kukuza shughuli za kilimo nchini.
Katika ziara yake mkoani Morogoro, Rais Dkt. Samia alihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM Ifakara, Wilaya ya Kilombero. Rais alisisitiza umuhimu wa kuimarisha hali ya maisha ya wakulima na kuendelea kuweka mkazo kwenye maendeleo ya kilimo, kilicho muhimu kwa uchumi wa taifa.
Rais Samia amesisitiza kwamba maagizo haya ni sehemu ya mpango wa Serikali kupitia wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha ununuzi wa mpunga unafanyika kwa bei mpya ya shilingi 900 kwa kilo. Hatua hii inalenga kuhakikisha wakulima wanapata bei bora kwa mazao yao na hivyo kuboresha kipato chao.
Kwa mujibu wa Rais, ongezeko hili la bei linakuja ili kuimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata faida inayostahili kutokana na jasho lao na gharama wanazopata katika uzalishaji wa mpunga.
#KonceptTvUpdates