Kaimu katibu tawala sekta za uchumi na uzalishaji Mkoani Iringa, Mwita Chacha amewatoa hofu ya kukosa elimu Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ambao hawajapata nafasi ya kuhudhuria maonesho ya nanenane 2024 kanda ya nyanda za juu kusini kwa kusema kuwa elimu ya sekta hizo inatolewa katika ofisi zote za Halmashauri za mkoa wa Iringa.
Chacha ameyasema hayo leo Agosti 05, 2024 wakati akizungumza na Shamba Fm kwa njia ya simu kutokea viwanja vya John Mwakangale Mkoani Mbeya ambapo maonesho hayo yameanza kutoka Agosti Mosi na kilele chake kufanyika Agosti 08, 2024.
Katika hatua nyingine Chacha amesema kuwa maonesho ya nanenane ya 2024 kanda ya nyanda za juu kusini yanaendelea kufanyika vizuri kwa kuhakikisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliohudhuria katika maonesho hayo wanajifunza namna mbalimbali za kukuza shughuli zao wanazozifanya na kuzipa thamani zaidi.
“kwa kiasi kikubwa Wananchi ambao wanatembelea mabanda ya kilimo, mifugo na uvuvi kutokea mkoani Iringa wanauliza ni zipi teknolojia wezeshi katika shughuli zao za kilimo, uvuvi na ufugaji wanazoweza kuzitumia ili kuongeza ubora na tija zaidi na tunawahakikishia Wakulima kanda ya nyanda za juu kusini kuwa endapo watahudhuria katika maonesho hayo watapata faida nyingi ukitoa kilimo, uvuvi na ufugaji kwani sekta na taasisi za serikali na binafsi zipo nyingi na zinatoa elimu na huduma mbalimbali za kijamii”, amesema Chacha.