Tanzania inatarajiwa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Kituo cha Umahiri cha Matibabu, mradi mkubwa unaotekelezwa na African Export-Import Bank (Afreximbank) kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha King, iliyoko London, Uingereza. Hospitali hii itakuwa na viwango vya dunia na inatarajiwa kuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 500 kwa wakati mmoja, ikitoa huduma za kisasa kwa magonjwa ya kansa ya damu na sickle cell.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Kimatibabu, Abuja, Bw. Brian Deaver, alieleza kuwa teknolojia itakayotumika katika hospitali hii ni ya kisasa na haijawahi kutumika katika Bara la Afrika. Hospitali hiyo, pamoja na hospitali nyingine zitakazojengwa nchini Ghana, Kenya na Tanzania, zitatoa huduma mtambuka kama uchunguzi, matibabu, tiba kwa njia ya nyuklia, upasuaji, na huduma baada ya upasuaji.
Bw. Deaver alisema, “Tunapotekeleza mradi huu tunalenga kutoa huduma bora za afya, kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya, kufanya utafiti, kutoa ajira, kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni na kukuza utalii wa kimatibabu kwa nchi za Afrika.”
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea mradi huo nchini Nigeria, alisema kuwa mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa huduma za matibabu kwa Watanzania. Hata hivyo, pia alikiri kwamba utekelezaji wa mradi huo unakabiliwa na changamoto za kifedha na za usimamizi ambazo zinaweza kuathiri muda wa kukamilika kwa mradi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, aliunga mkono kauli ya Waziri Nchemba, akisema, “Mradi huu ni mfano wa jinsi tunavyoweza kuimarisha sekta ya afya nchini Tanzania na pia kuongeza nafasi ya Tanzania kama sehemu ya utalii wa kimatibabu.”
Hayo yamejili wakati Dkt. Nchemba alipoongoza ujumbe wa Tanzania, ukiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, ambao walishiriki katika Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings) iliyowashirikisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Bi. Judica Nagunwa, alisema kuwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimekuwa zikilenga kuimarisha afya za Watanzania. Alisisitiza kuwa ubalozi wake utaendelea kufanya kazi kwa karibu kuhakikisha mradi unafanikiwa.
Afreximbank, taasisi ya fedha ya kimataifa inayojihusisha na kuendeleza biashara barani Afrika, itatoa ufadhili wa zaidi ya dola za Marekani milioni 260 kwa ajili ya mradi huu.
#KonceptTvUpdates