Kanisa la mchungaji Paseka Mboro Motsoeneng wa Afrika Kusini limechomwa moto kufuatia video yake akiwachukua watoto kwa nguvu katika Shule ya Msingi ya Matsediso huko Katlehong Ekurhuleni jana.Haijulikani ni nani au ni nini chanzo cha moto huo.
Mchungaji Mboro alizua taaruki jana Jumatatu Agosti 05, 2024 baada ya katika Shule ya Msingi ya Matsediso kumfata mjukuu wake kwa nguvu, akiwa na panga na kutishia kuwashambulia walimu huku bodigadi mwenye bunduki akiwa karibu.
Baba wa mtoto huyo akionekana kuwashika watoto wake wawili. Mama wa watoto hao alifariki Aprili 2024 na kuacha mzozo kati ya familia upande wa baba na wa mama kuhusu malezi ya watoto.
Siku ya tukio, baba wa watoto hao alikuwa na kikao na mkuu wa shule asubuhi. Baadaye mchana bibi mzaa mama naye alikutana na mkuu wa shule na akamjulisha juu ya mgogoro uliotokea katika kikao cha familia cha hivi karibuni.
Bibi akadai upande wa baba wameshindwa kulea vizuri watoto, baba nae alivyoenda kuchukua watoto wake baada ya masomo, uongozi wa shule ukakataa, ukidai mpaka bibi atoe idhini.
Familia ya upande wa baba ikiongozwa na Pastor Mboro hawakupenda jinsi familia upande wa mama inavyotaka kuishi na watoto kwa nguvu.
Hii ilisababisha mchungaji huyo kufika shuleni akiwataka wajukuu kwa nguvu.
“Hata wanafunzi wa Yesu walikuwa na mapanga. Sio kosa wachungaji kuwa na walinzi wanaobeba mitutu ya bunduki.” – amesema Mboro.
Mamlaka ya Elimu ya Gauteng imelaani kitendo hicho na taratibu za awali za kusululisha mgogoro huo zinaendelea.