Taarifa iliyotolewa na chama cha ACT Wazalendo inasema ” ACT WAZALENDO inalaani vikali tukio la ubakaji lililofanywa na vijana watano huku wakichukua picha za video na kutuma kwenye mitandao ya kijamii”
Taarifa zilizosambaa mitandaoni kuanzia Agosti 2, 2024 ziliwaonesha vijana hao wakimwingilia binti huyo kwa kupishana na kinyume na maumbile. Matukio ya kinyama dhidi ya wanawake na watoto yameshika kasi ndani ya nchi yetu huku jeshi la polisi likijivuta kuchukua hatua kwa wahalifu hao.
Tukio hili ni mwendelezo tu, kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi kwa mwaka 2023 makosa dhidi ya binadamu na makosa dhidi ya maadili ya jamii yalikuwa 28,769.
Hii ni ishara kuwa matukio ya ukatili yanazidi kukithiri nchini kwetu. Aidha, taarifa zinaonyesha kuwa vijana hao ni askari wa jeshi la polisi na aliyehusika kuandaa unyama huu ni askari wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama.
Kwamba amefanya jambo hilo kutokana na wivu wa mapenzi. Tunaungana na wadau wengine kulaani matendo haya yanayozidi kushamiri na kutaka hatua zichukuliwe haraka.
Kitendo cha watu hao kupata ujasiri wa kubaka na kurekodi na kutuma mtandaoni ni ishara kuwa mamlaka husika zinalegalega. Kutokana na kuendelea kwa matukio ya ubakaji, utekaji, utesaji na ukamatwaji wa wanachi kinyume na sheria, ACT Wazalendo tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Ndg. Hamadi Masauni ajiuzulu mara moja kwa kushindwa kazi.
Mwisho, tunalitaka Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi haraka juu ya tukio hilo na wahusika wote katika tukio hilo wachukuliwe hatua za kisheria.
Imetolewa na;Ndg. Janeth Joel Rithe.
Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu.
ACT Wazalendo
06 Agosti, 2024.