Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) imelaani vikali kitendo cha ukatili wa kijinsia kilichoripitiwa kumhusu msichana mmoja mkazi wa Dar es Salaam, Wilaya ya Temeke katika Kata ya Makangarawe anayedaiwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia baada ya picha zake kusambaa mitandaoni akifanyiwa vitendo vya kidhalilishaji na takribani vijana watano.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda leo Agosti 6, 2024 imeeleza kuwa Vitendo vya ulawiti, ubakaji na udhalilishaji kama huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na vinaleta athari zinazodumu kwa muda mrefu kwa wahanga na ni kinyume na sheria na hakipaswi kuvumiliwa hata kidogo.
UWT imesisitiza Uchunguzi wa kina na uwajibikaji wa haraka kutoka katika mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha haki inatendeka na watuhumiwa wanafikishwa katika vyombo vya sheria.
Pia, Msaada wa kisaikolojia unapaswa kutolewa haraka iwezekanavyo kwa mhanga wa tukio hili.
“Watanzania wote tuna wajibu wa kulinda taswira ya nchi yetu kwa kukemea vikali matukio ya udhalilishaji na ukatili wa aina yoyote ile pamoja na kutunza mila na desturi zetu. Tanzania isiyo na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia inawezekana” – Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda