Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi, katika Ikulu ya Zanzibar. Mazungumzo hayo yalifanyika kwa lengo la kuleta salamu na mwaliko kutoka kwa Mhe. Sheikha Moza Bint Nasser, Mwenyekiti wa Taasisi ya Qatar Foundation.
Katika mkutano huo, Balozi Al Marekhi alimkabidhi Rais Mwinyi mwaliko rasmi wa kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Maadhimisho ya Miaka 30 ya Qatar Foundation, linalohusu Familia na masuala ya Utandawazi. Kongamano hili linatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2024 na litawaleta pamoja viongozi na wataalamu mbalimbali kujadili changamoto na fursa zinazoikabili familia katika enzi za utandawazi.
Rais Mwinyi alieleza furaha yake kwa mwaliko huo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Qatar katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, na maendeleo ya kijamii. Aidha, aliongeza kuwa ushiriki wa Zanzibar katika kongamano hilo utatoa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mengine.
#KonceptTvUpdates