Idara ya Sanaa na Utamaduni Zanzibar, imesema imeanza kuchukua hatua kali kwa madereva ambao wanaweka muziki katika gari zao (mabasi) wakati wanapokwenda harusini au katika shughuli za michezo na kuwaruhusu wanawake kukata mauno ndani ya gari wakati zinatembea barabarani.
Kamishina wa Idara hiyo, Dkt Omar Mohammed Salum amesema kufanya hivyo ni kinyume na mila, na desturi za utamaduni wa Mzanzibari na tayari wameanza kutoa elimu juu ya kuwataka baadhi ya madereva kuachana na mambo hayo haraka.
“Utaikuta Gari imewekwa muziki na akina mama wanacheza wengine wamepanda juu ya viti wanakata mauno na kunyanyua vijora vyao juu kuonesha maungo yao, jambo ambalo ni kinyume hasa na utamaduni wetu, kwa kweli hili linatumiza vichwa kwani vizazi vyetu vya baadae vitarithi kitu gani.
Ili kufanikisha hilo tunaiomba jamii kuendelea kutoa mashirikiano katika kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wahusika na kuondosha janga hili linakazi.” amesema Dkt Omar.
“Hawa wanawake wanaokodiwa kwenda kucheza kwenye viwanja vya michezo kwa kweli ni mitihani kwani wanakuwa hawajielewi huu sio utamaduni wetu.”