Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, na Soko la Bidhaa Tanzania imetoa mwongozo mpya wa biashara ya mbaazi na dengu kwa msimu wa 2024/2025. Mwongozo huo, Toleo la 3-2024, umelenga kulinda ubora wa mazao na kuongeza ushindani katika minada.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Chakula Sura 249 na marekebisho ya Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Sura 274, mwongozo huu unasisitiza umuhimu wa mnunuzi kujisajili na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mchanganyiko kupitia kiunganishi maalum. Mnunuzi anapaswa kuwasilisha nyaraka muhimu kama vile Usajili wa Kampuni, Cheti cha Kuandikishwa, Utambulisho wa Namba ya Mlipa Kodi (TIN), Certificate of Tax Clearance, Leseni ya Biashara, na Namba ya NIDA.
Mwongozo pia unaelekeza utaratibu wa uendeshaji wa minada kwa mbaazi na dengu, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji kupitia vyama vya ushirika, stakabadhi ghalani, na mauzo ya minada ya kielektroniki yanayoendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
COPRA imetangaza kuwa minada ya mbaazi na dengu itafanyika kila wiki katika mikoa husika, na ratiba ya minada itatangazwa kupitia tovuti ya COPRA na kurasa zake za mitandaoni. Mwongozo huu unapatikana kwenye tovuti ya COPRA kupitia kiunganishi https://www.copra.go.tz/publications/guidelines.
Hatua hii ina lengo la kuhakikisha kwamba wakulima na wafanyabiashara wanapata bei nzuri kwa mazao yao kupitia mfumo wa minada ambao unatoa ushindani wa haki na uwazi. Pia, inalenga kuongeza ubora wa mazao na kuhakikisha kwamba mazao yanayouzwa yanakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa.
#KonceptTvUpdates