Mhandisi Mkama Bwire, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ameeleza mafanikio na changamoto zinazokabili mamlaka hiyo katika uzalishaji wa maji safi kwa jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine inayohudumiwa. Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo, Jumatano Agosti 07, 2024, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Bwire alitoa muhtasari wa hali ya uzalishaji wa maji na mahitaji yake yanavyoendelea kuongezeka.
Mhandisi Bwire alifafanua kuwa mitambo na vyanzo vya maji vinavyotumiwa na DAWASA vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 534,600 kwa siku, sawa na lita 534,600,000 kwa siku. Uzalishaji huu mkubwa unalenga kukidhi mahitaji ya wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa na DAWASA kama vile baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro, Pwani, na Tanga. Hata hivyo, mahitaji ya maji katika maeneo haya yanazidi kuongezeka kila siku, hasa kutokana na upanuzi wa huduma za DAWASA.
“Lakini kwa takwimu hadi tunafika mwaka jana (2023) tulikuwa na mahitaji karibu mita za ujazo laki 5 na elfu 44, kwa hiyo ukiangalia katika takwimu hii (kwa sababu tumekuwa tukireview kila baada ya mwaka) naamini mwaka huu tukifika mwishoni inaweza kuwa imeongezeka sana hususani kutokana na maeneo ya huduma yanayoongezeka hususani kwenye mkoa wa Pwani inaweza kuwa kubwa sana,” alisema Mhandisi Bwire. Aliongeza kuwa kwa mwaka jana, mahitaji yalifikia mita za ujazo 504,000 kwa siku, na hivyo kuzalisha pengo la mita za ujazo 10,000 kati ya uzalishaji wa mitambo na mahitaji.
Mhandisi Bwire alieleza kuwa, kwa kuzingatia mwenendo wa ongezeko la mahitaji, mamlaka hiyo inafanya juhudi za kuongeza uzalishaji wa maji ili kukidhi mahitaji hayo. Hii inajumuisha kuboresha na kupanua mitambo iliyopo pamoja na kutafuta vyanzo vipya vya maji.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, ambao walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi zaidi kuhusu mikakati ya DAWASA katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa. Mhandisi Bwire aliwahakikishia wahariri na umma kwa ujumla kuwa DAWASA itaendelea kujitahidi na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma zake na kukidhi mahitaji ya maji safi kwa wananchi.
#KonceptTvUpdates