Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza umetoa tahadhari kwa Watanzania wote wanaoishi nchini humo kufuatia vurugu zinazoendelea katika maeneo mbalimbali. Katika tangazo lililotolewa na ubalozi huo, Watanzania wamehimizwa kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ili kujiepusha na hatari inayoweza kujitokeza kutokana na vurugu hizo.
Tangazo hilo limeeleza kuwa ubalozi uko tayari kusaidia endapo kutatokea hali ya dharura, na utaendelea kutoa msaada kwa Watanzania hadi hali itakapokuwa shwari. Ubalozi umesisitiza umuhimu wa kuwasiliana nao kwa njia ya barua pepe au simu ili kupata msaada au taarifa zaidi kuhusu usalama wao.
Kwa mawasiliano, Watanzania wanaweza kutumia barua pepe zifuatazo: tanzania@tzhc.uk na ubalozi@tzhc.uk. Vilevile, mawasiliano ya simu yanapatikana kupitia namba +44 20 7569 1470, +44 7880 870 540, na +44 7909 323 286.
Tangazo hili limekuja wakati ambapo vurugu na machafuko yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo kadhaa nchini Uingereza, na hivyo kuchukua tahadhari ni muhimu kwa usalama wa raia wote. Ubalozi umehitimisha kwa kuwashukuru Watanzania kwa ushirikiano wao na kuwatakia hali ya usalama katika kipindi hiki kigumu.
#KonceptTvUpdates