Msimu wa ununuzi wa mbaazi na dengu kwa mwaka 2024/2025 umezinduliwa rasmi tarehe 07 Agosti 2024 nchini Tanzania. Uzinduzi huo umefanyika katika ghala la Gendi, Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoa wa Manyara, ambapo mnada wa kwanza kitaifa umefanyika mapema jana saa 4:00 asubuhi.
Hii ni hatua muhimu katika kukuza sekta ya kilimo nchini na kuhakikisha ubora wa mazao. Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, na Soko la Bidhaa Tanzania imeandaa mwongozo wa biashara ya mbaazi na dengu. Mwongozo huu, Toleo la 3-2024, unalenga kulinda ubora wa mazao na kuongeza ushindani kupitia minada.
Mamlaka imesisitiza kwamba mnunuzi yeyote wa mbaazi na dengu anapaswa kujisajili kupitia tovuti ya COPRA na kuambatisha nyaraka muhimu kama vile Usajili wa Kampuni, Cheti cha Kuandikishwa, Utambulisho wa Namba ya Mlipa Kodi (TIN), Certificate of Tax Clearance, Leseni ya Biashara, na Namba ya NIDA.
Kwa mujibu wa mwongozo, minada ya mbaazi na dengu itafanyika kila wiki katika mikoa husika, na ratiba ya minada itatangazwa kila wiki kupitia tovuti na kurasa za mitandaoni za COPRA.
#KonceptTvUpdates