Saa chache zikiwa zimebaki kabla ya kupigwa pambano la Watani wa Jadi nchini, Msemaji wa Yanga SC Haji Manara amesema hatoenda uwanjani kutazama pambano hilo.
Manara amesema atautazama mchezo huo katika luninga akiwa nyumbani kwake, lakini sio kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kutakapopigwa pambano hilo.
“Siendi uwanjani. Mimi bwana tangu mechi hizi kubwa zianze kuoneshwa katika luninga nimekwenda mechi chache. Hivi umewaza tukifungwa itakuwaje? Mimi sitazimia, nitakufa kabisa. “Maana mkifungwa jiandae kuona unachorwa vikalagosi, Social Media.
“Muone mtu kama yule Msemaji wa Simba SC ( Ahmed Ally) hivi atakuwaje timu yake ikipoteza? alihoji Manara. Manara alikwenda mbali na kusema huwa anapenda kuwaandaa kisaikojolia mashabiki wao ikitokea mambo yamekuwa tofauti.
Leo Agosti 8 michezo ya Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii itapigwa, Saa 10 : 00 Jioni, utapigwa mchezo kati ya Azam FC na Coastal Union katika uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar
Baadaye majira ya Saa 1 :00 Usiku watani wa jadi Simba na Yanga watavaana katika Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.