Ally Masoud Nyomwa, maarufu kama Masoud Kipanya, mchoraji wa katuni na mtangazaji maarufu nchini Tanzania, amefungua kesi ya kashfa dhidi ya Burton Mwemba, anayejulikana kama Mwijaku. Kipanya anamtuhumu Mwijaku kwa kumshushia hadhi na heshima kupitia maandishi yaliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kesi hiyo, iliyosajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Ndogo ya Dar es Salaam) tarehe 05 Agosti 2024, itasikilizwa na Jaji David Ngunyale kuanzia tarehe 03 Septemba 2024. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili wa Kipanya, Alloyce Komba, Mwijaku ameshapokea wito wa kufika mahakamani na anatakiwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya siku 21.
Kipanya anadai kuwa mnamo tarehe 04 Juni 2024, Mwijaku alichapisha maneno ya kashfa kupitia akaunti zake za Facebook na Instagram, akidai Kipanya anahusika na biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana nchini, na kwamba anawadhalilisha viongozi wa serikali kwa malipo ya hongo.
Kutokana na madai hayo, Kipanya ameiomba mahakama imwamuru Mwijaku kulipa fidia ya Shilingi milioni 500 kwa madhara halisia na Shilingi bilioni tano kwa madhara ya jumla. Pia ameomba malipo ya kiadhabu na riba ya asilimia 31, pamoja na amri ya kumtaka Mwijaku kuomba radhi hadharani na kuondoa maandishi ya kashfa mtandaoni.
Kesi hii imezua mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakijiuliza iwapo mashtaka ya kashfa yanaweza kuathiri namna watu wanavyotoa maoni yao mtandaoni. Ikiwa Kipanya atashinda kesi hii, inaweza kuwa na athari kubwa kwa watumiaji wa mitandao na jinsi wanavyojieleza kuhusu masuala mbalimbali, hasa kuhusu viongozi na watu maarufu.
#KonceptTvUpdates