Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Maabara ya Taifa ya Kilimo, ikiwa ni sehemu ya mradi mkubwa unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Hafla hiyo imefanyika jijini Dodoma, katika viwanja vya Nzuguni, ambako maabara hiyo itajengwa.
Maabara hii itajumuisha maabara 14 na itakuwa kitovu cha tafiti za kilimo nchini, ikiwemo makao makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Hatua hii ni muhimu kwa sababu maabara hii itakuwa ya rufaa kwa vituo vyote vya utafiti wa kilimo nchini, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutumia sayansi na teknolojia za kisasa.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, alieleza kuwa maabara hizo zitakuwa na ofisi 14 za utawala ili kurahisisha utendaji kazi. Aidha, alisema kuwa serikali inafanya juhudi za kuongezea mradi huu eneo zaidi ili kuongeza ukubwa na uwezo wa maabara hiyo.
“Kukamilika kwa mradi huu kutachochea uzalishaji wa miche na teknolojia, ambapo mwaka huu tutajenga maabara ya Bio-Science na vituo vya Horticulture mkoani Arusha, ambavyo vitakuwa na maabara kubwa ya Tissue Culture,” alisema Mhe. Bashe.
Mradi huu unatarajiwa kubadilisha sura ya sekta ya kilimo nchini, hasa katika kuhakikisha kuwa tafiti zinafanyika kwa kiwango cha juu na kutoa suluhisho kwa changamoto za kilimo nchini Tanzania.
Rais Samia alikuwa jijini Dodoma kwa ajili ya kushiriki katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, maarufu kama NaneNane, ambapo miradi ya kilimo kama huu unaochochea maendeleo endelevu ilikuwa moja ya masuala muhimu yaliyosisitizwa.
#KonceptTvUpdates