Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema kuwa Serikali inaandaa utaratibu rasmi wa kutambua mchango wa vijana wanaojitolea kwenye taasisi mbalimbali za serikali. Sangu ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Kata ya Ikozi na Kalambanzite, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Katika hotuba yake, Sangu alisisitiza kuwa utaratibu huu utasaidia kuwapata vijana sahihi wanaojitolea badala ya kupata mamluki ambao hupenyezwa na ndugu zao pindi fursa za ajira zinapojitokeza. “Tunaandaa utaratibu ambao utasaidia kutambua na kuthamini mchango wa vijana wanaojitolea katika taasisi za serikali, na hivyo kuepuka udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wenye ndugu zao,” alisema Sangu.
Aliongeza kuwa udanganyifu huo umekuwa ukipelekea manung’uniko miongoni mwa vijana sahihi wanaojitolea kwa uaminifu na bidii. “Utaratibu huu utakuwa mwarobaini wa namna bora ya kutambua na kuthamini mchango wa vijana hawa,” alibainisha Naibu Waziri.
Katika hatua nyingine, Sangu alizungumzia juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hata hivyo, alielezea wasiwasi wake juu ya baadhi ya watumishi wasiowaaminifu wanaofuja fedha hizo.
“Rais wetu amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini kuna watumishi wasiowaaminifu ambao wameanza kufuja fedha hizo. Kufuatia hatua hiyo, natoa wito kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwabana watumishi hao ili kukomesha tabia hiyo,” alisema Sangu.
Sangu alisisitiza kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuwasimamia watumishi wote nchini ili kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. “TAKUKURU hakikisheni mnawabana watumishi ambao ni wadokozi wa fedha za miradi ya maendeleo inayotolewa na Rais wetu,” alihitimisha Sangu.
#KonceptTvUpdates