Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitoa wito kwa Watanzania kuruhusu miradi ya maendeleo kupita kwenye viwanja na mashamba yao, huku serikali ikiahidi kulipa fidia baadaye. Hata hivyo, kauli hii imeibua maoni tofauti kutoka kwa wananchi na wataalamu wa sheria.
Wakili wa kujitegemea, Fatma Karume, alitoa maoni yake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X. Karume alieleza kuwa serikali inayojali maendeleo hupanga fidia ya bomoabomoa katika bajeti ya miradi ya miundombinu. Alisisitiza kuwa bila pesa za fidia, maendeleo hayo hayawezi kupatikana kwa haki.
“Serikali makini na inayojali maendeleo huweka fidia ya bomoabomoa kwenye bajeti ya kujenga miundombinu. Kama hamna pesa za fidia, hatuwezi kuwa na uwezo wa kupata hayo maendeleo! Tusijenge miundombinu kwa kuumiza na kuwarejesha nyuma wachache! Hiyo si haki! Ni dhuluma!” alisema Karume.
Akirejea Ibara ya 24(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Karume alieleza kuwa inakataza kuchukuliwa kwa mali ya mtu bila ya kupewa fidia. Aliongeza kuwa malipo ya fidia ni haki ya msingi na yanapaswa kulipwa haraka ili kuepusha madhara kwa wananchi.
“Jamani nchi hii hatutoi wenzetu kafara ili tupate maendeleo na wao waangamie kimaisha. Malipo ya fidia ni haki yao na zilipwe haraka hata pale serikali inabomoa nyumba ili tupate barabara. Kweli barabara yetu sote iumize watu wachache?” alihoji Karume.
Wakili huyo alisisitiza umuhimu wa kufanikisha maendeleo kwa haki na kutokumuumiza mtu yeyote. Alibainisha kuwa kila Mtanzania anayevunjiwa nyumba au kuchukuliwa shamba ana haki ya kulipwa fidia kwa wakati. “Nchi ya haki haijengi barabara ikavunja nyumba na kuacha watu bila makazi, hayo si maendeleo! Ni dhulma! Walipwe fidia zao papo hapo. Nyumba ni maendeleo kwa mtu binafsi, unamvunjia maendeleo yake bila ya fidia halafu unasema nitakuletea maendeleo ya wengi,” alisema Karume.
Kauli hizi zimeibua maoni tofauti kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Wengine wameonyesha kuunga mkono msimamo wa Karume, wakisisitiza umuhimu wa kulipa fidia kabla ya kuanza kwa miradi ya maendeleo. Serikali bado haijatoa tamko rasmi kuhusu maoni haya ya Wakili Fatma Karume, na mjadala unaendelea kuhusu njia bora ya kufanikisha maendeleo huku haki za wananchi zikiheshimiwa.
#KonceptTvUpdates