Kijana aliyefahamika kwa jina la Shalom Tarimo (21) amefariki dunia leo, Agosti 9, 2024, wakati akifanya usafi katika kituo cha mafuta cha Uhuru Peak, mjini Moshi. Tarimo, ambaye alikuwa mfanyakazi katika kituo hicho, alipoteza maisha baada ya kutumbukia kwenye kisima cha mafuta wakati akijaribu kuokota simu iliyodondoka kutoka mfukoni mwake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Tarimo alikuwa akifanya shughuli za usafi katika eneo la kisima cha mafuta kilichopo katika kituo cha Total Energies cha Uhuru Peak, wakati ajali hiyo ilipotokea. Simu yake iliteleza kutoka mfukoni, na alipokuwa akijaribu kuirejesha, alijikuta akitumbukia kwenye kisima hicho.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliwasili haraka eneo la tukio na kufanya jitihada za kumuokoa Tarimo. Hata hivyo, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa, iliwachukua takribani saa moja kutoa mwili wake kutoka kwenye kisima hicho.
Tukio hili limetia simanzi kwa wafanyakazi wenzake na wakazi wa Moshi, huku likisisitiza umuhimu wa tahadhari wakati wa kazi katika mazingira hatarishi.
#KonceptTvUpdates