Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na maafisa waandamizi wa benki hiyo, walifanya ziara maalum katika banda la Serengeti Breweries Limited kwenye viwanja vya Nane Nane mjini Dodoma leo. Ziara hiyo ililenga kujionea na kujifunza zaidi kuhusu shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo katika uzalishaji wa bia, hasa kupitia mazao wanayonunua moja kwa moja kutoka kwa wakulima nchini.
Katika ziara hiyo, Nsekela alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa Serengeti Breweries kuhusu mchango wa kampuni hiyo katika kuinua sekta ya kilimo nchini. Alisema kuwa ushirikiano kati ya benki ya CRDB na Serengeti Breweries ni muhimu, hasa katika kuwezesha wakulima kupata masoko ya uhakika kwa mazao yao, ambayo hutumika kama malighafi muhimu katika uzalishaji wa bia.
Viongozi wa Serengeti Breweries walieleza kuwa kampuni hiyo inajivunia kutumia zaidi ya asilimia 70 ya malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa bia kutoka kwa wakulima wa ndani. Hii ni sehemu ya mkakati wao wa kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Ziara hii inakuja wakati ambapo maonyesho ya Nane Nane yanaendelea kuvutia maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakijionea teknolojia na mbinu mpya za kilimo, pamoja na fursa za biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali.
#KonceptTvUpdates