Producer maarufu Mazuu wa Mazuu Records amefunguka kuhusu changamoto kubwa alizokutana nazo wakati wa safari ya muziki ya msanii Rich Mavoko, akisisitiza kuwa licha ya mafanikio, kulikuwa na vikwazo vingi ambavyo vilihitaji uvumilivu na juhudi kubwa.
Mazuu, akizungumza kwenye kipindi cha *Planet Bongo* cha East Africa Radio, alieleza kuwa moja ya nyimbo ambazo zilikutana na changamoto kubwa ni “Roho Yangu.” Alifichua kuwa kulikuwa na juhudi za makusudi za kuzuia wimbo huo usichezwe kwenye redio mbalimbali nchini, jambo lililosababisha wao kama timu yake kukaa vikao vingi na kutumia fedha nyingi kutatua tatizo hilo.
“Ngoma ambayo ilitusumbua sisi ni ‘Roho Yangu,’ iliwekewa hadi vikao na hela ili isipigwe redio zote. Mimi na meneja wa Mavoko tuliumiza kichwa sana, hadi tukasema tutoe ngoma nyingine ya pili,” alisema Mazuu.
Baada ya kukutana na vikwazo hivyo, Mazuu na timu yake waliamua kutoa wimbo mwingine uitwao “Pacha Wangu.” Alifafanua kuwa wadau walijitokeza kusaidia, ambapo kiasi cha Shilingi milioni 40 kilitolewa kwa ajili ya kurekodi na kufanya promosheni ya wimbo huo mpya.
Mazuu pia alifafanua jinsi ambavyo kipindi hicho, Rich Mavoko alikuwa na umaarufu mkubwa kuliko hata Diamond Platnumz, lakini alikumbana na shinikizo kubwa kutoka lebo ya WCB ili ajiunge nao. Alieleza kuwa WCB walimpa Mavoko machaguo mawili: kujiunga nao au aachane kabisa na muziki. “Rich Mavoko alikuwa amekataa kujiunga na WCB, ilibidi nimuombe sana kwa sababu vita ya WCB ilikuwa kubwa,” alisema Mazuu.
Akitupia macho nyuma, Mazuu alisisitiza kuwa haikuwa nia ya Mavoko kujiunga na WCB, bali lebo hiyo ndiyo ilitaka msanii huyo waandamane nao kwa sababu ya kipaji chake kikubwa na uwezo wa kuimba katika aina yoyote ya muziki.
Mazuu aliendelea kuelezea jinsi Mavoko alivyokuwa msanii ambaye ni mtoto msumbufu kuliko Kiba, lakini mwenye uwezo wa kipekee wa kuimba kwa namna yoyote, jambo ambalo lilimfanya kuwa kipenzi cha wengi.
Hii inaonyesha changamoto zinazowakumba wasanii na timu zao katika safari ya kutafuta mafanikio kwenye muziki, na jinsi gani vipaji vyao vinavyoleta mvutano ndani ya tasnia.
#KonceptTvUpdates