Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetoa taarifa ya kusikitishwa na kulaani vitendo vya Wananchi kupotea katika mazingira tatanishi, kutekwa na kuteswa na baadae kuonekana huku baadhi yao wakiwa wamefariki na wengine wakiwa na majeraha makubwa katika miili yao hali inayotia hofu kwa wananachi juu ya usalama wao na mashaka juu ya uwezo wa Jeshi la Polisi kuchunguza na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wa matukio hayo.
Taarifa ya Baraza la Uongozi la TLS imeeleza kuwa “TLS inatambua na kuheshimu taarifa za Jeshi la Polisi zinatolewa zikitaarifu umma kwamba matukio hayo yamekuwa yanafanyiwa uchunguzi lakini tunasikitika kwamba hakuna taarifa kamili ya uchunguzi wa tukio hata moja ambayo imewahi kutolewa kwa umma juu ya hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi juu ya watuhumiwa wa matukio hayo.
“Tunasikitishwa pia na namna ambavyo vyombo vyetu vya dola hususani Jeshi la Polisi limekuwa likifanyia kazi taarifa hizo. Mara kwa mara Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha kutokea kwa matukio hayo lakini baadae inakuja kubainika kwamba matukio hayo ni ya kweli.” imesema taarifa ya TLS.
“Mara nyingine Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata raia wema wanaotoa taarifa hizo kwa kile kinachosemekana kusambaza taarifa za uongo badala ya kufanyia kazi taarifa hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria zinazowapasa kufanya wajibu wao wa kulinda watu na mali zao.”
TLS imevikumbusha vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi juu ya majukumu yake ya Kikatiba na Kisheria ya kulinda watu na mali zao matukio haya ya utekaji ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mikataba ya Kimataifa juu ya Haki za Binadamu na inayozuia uteswaji wa watu.
Aidha TLS imemshauri Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda Tume maalumu ya kuchunguza matukio yote ya kupotea kwa watu, kutekwa na kuteswa pamoja na kuunda Tume Maalum ya kuchunguza ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye masuala ya Utekaji kwa kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa kushiriki katika vitendo hivyo.
“Tunapendekeza kuundwa kwa chombo maalumu cha kudumu cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola (oversight body) ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria.”