Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa asilimia 100 kunalenga kukipatia ushindi wa kihistoria chama hicho katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo tarehe 09 Agosti 2024, wakati akizungumza na makundi ya hamasa ya CCM katika ukumbi wa mikutano wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Mjini Magharibi, Unguja.
Dk. Mwinyi amekiri mafanikio makubwa yaliyopo katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Uwekezaji, Mawasiliano, Uwezeshaji na Miundombinu. Ameyataka makundi ya hamasa ya Chama hicho kuelezea mafanikio hayo kwa wananchi.
Eneo jingine aliloliwekea mkazo ni kwa wanachama wa CCM kujipanga tayari kwa Uchaguzi Mkuu ujao pamoja na kuwahamasisha wananchi kuipigia kura CCM.
Akizungumzia uwezeshaji kwa wananchi, Makamu Dk. Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imedhamiria kuwafikia wananchi wote ambao bado hawajapata fursa za uwezeshaji.
Dk. Mwinyi amewahimiza wana CCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakapoanza mapema mwezi Januari mwakani.