Zaidi ya shilingi bilioni 145.7 zinatumika kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda katika Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.
Mradi huo unategemewa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 490,926 wa vijiji 60 .
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) imepewa taarifa na Msimamizi wa mradi Mha. Betty Kaduma ambaye amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 45.5.
Mha.Kaduma ameongeza kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha majisafi kutoka Tabora Mjini hadi katika Miji ya Sikonge, Urambo/Kaliua kwa jumla ya kilomita190.169. Kazi zingine ni pamoja na ujenzi wa matangi matano ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita kati ya 1,000,000 na 2,000,000.
Msimamizi huyo wa mradi ameongeza kuwa Mkandarasi M/S Megha Engineering Infrastucture Limited ambaye ndiye anayetekeleza mradi huo anatakiwa kuongeza kasi ya utekelezwaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kama ilivyopangwa Oktoba 2025.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KASHWASA Mha. Joshua Mgeyekwa ameelezea kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na hatua uliofikia hadi sasa.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi amemtaka Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi huo kuhakikisha anazingatia ubora na kuukamilisha kwa muda uliopangwa.