Na Mwandishi Wetu, Arusha
KAMPUNI ya Oryx Gas imekabidhi mitungi 600 ya oryx ya kupikia kwa familia zenye watoto wenye ulemavu mkoani Arusha ambapo ni katika jitihada za kumuunga mkono Mbunge wa Arusha Vijijini, Mrisho Gambo.
Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na Mbunge huyo kwaajili ya kugawa vifaa saidizi kwa watoto wenye ulemavu Jijini Arusha jana, Meneja Masoko wa Orxy Gas Peter Ndomba amesema msaada huo ni sehemu ya misaada mbalimbali ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiitoa kwa familia duni nchini lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuokoa mazingira yetu.
“Oryx tumekuwa tukishiriki kikamilifu katika kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za Rais DK.Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha matumizi ya nishati safi.Tumekuwa tukishirikiana na Wabunge mbalimbali katika kuwezesha wananchi kupata mitungi ya gesi ya Oryx na majiko yake bure.”
Akitoa elimu ya matumizi sahihi ya nishati ya gesi, Ndomba kabla ya kugawiwa kwa mitungi ya Oryx ,Ndomba amewatahadharisha watumiaji wa nishati hiyo kuwa makini na bidhaa hiyo kwa kutofunga milango wakati wa matumizi ili kuepuka athari kubwa endapo itatokea ikalipuka.
” Ukiwa nyumbani wakati unatumia gesi hakikisha milango Iko wazi ili hewa iweze kuingia na kutoka, lakini pia gesi yetu imetengenezwa kwa kuwekwa harufu kama yai viza, lengo ni kama ikatokea gesi ikavuja ni rahisi kusikia harufu tofauti na mtumiaji kuchukua tahadhari,” Amesema.
Kwa upande wake Mbunge Mrisho Gambo amewashukuru wadau mbalimbali kujitokeza kugawa vifaa pamoja na mitungi ya Oryx kwa familia zenye watoto wenye mahitaji Maalumu.
Akizungumzia msaada wa Orxy Gambo amesema kampuni hiyo imekuwa ikiendeshwa na watu waungwana kwa kuwa alipopeleka ombi lake walilifanyia kazi bila kuuliza maswali mengi tofauti na kampuni zingine.
” Nawashukuru Orxy kwa msaada huu wa mitungi ya gesi, nilivyoleta maombi kwenu mliyapokea kwa haraka lakini kampuni zingine zilianza kunihoji kwamba endapo tu kununua hawawezi, je gesi ikiisha wataweza kuijaza?, …jamani ndugu zangu kwani hapa mlipofikia mmekuwa mkiishi kwa misaada hii tu?,” Gambo aliwahoji wanufaika wa misaada hiyo.
Amesema mitungi hiyo itawarahisishia katika huduma ya nishati kwa kuwa wakati mwingine imekuwa ikiwawia ugumu sana kupata nishati ya kupikia kwa haraka hususani mtoto anapokuwa anasumbuliwa na maradhi na anatakiwa kupelekwa kupata huduma za Afya.
“Zoezi hili sio mara ya kwanza kulifanya hapa Arusha, tangu nimekuwa Mbunge mwaka 2000 tumekuwa tukigawa vifaa mbalimbali kwa walemavu lakini pia tumekuwa na utaratibu wa kusaidia kulipia bima ya Afya, namshukuru Rais Samia kwa kurejesha Bima kwa watoto, hii imesaidia sana,” amesema.
Amesema katika zoezi hilo la ugawaji wa vifaa tiba, Watoto 600 watapatiwa bima ya Afya ambapo kati yake yeye binafsi amelipia Watoto 210, mfanyabiashara Atul Mittal amelipia Watoto 100, Satbir HansPaul pamoja na marafiki zake Watoto 100 na Jiji la Arusha kupitia kwa mkurugenzi wake Juma Hamsini wamelipia Watoto 200.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Hamisi Hamduni amesema ofisi yake imeamua kumuunga mkono Mbunge huyo kwa kuwa kazi anayoifanya ni sadaka kwa Mungu lakini pia anatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
“Kwa kuwa kazi hii inayofanywa na Mbunge ni kazi ya Mungu sisi kama Jiji tunamuunga mkono na tunaahidi kulipia bima ya Afya Watoto 200 pamoja na baiskeli mwendo (wheel chair), tatu, hivyo Jumatatu nitakabidhi hundi ya milioni 11,” amesema.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel amempongeza Gambo kwa upendo wake anaoonyesha kwa wakazi wa Arusha na kumtaka kuendelea kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo kwa kuwa hilo ndio jambo la kwanza ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiliagiza kwa wateule wa Chama hicho.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu na kutibia magonjwa sugu ambayo awali yalikuwa hayatibiki nchini mpaka nje ya nchi na kwa gharama kubwa jambo ambalo lilisababisha watu wengi kupoteza maisha.