Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema kuwa Makamu Mwenyekiti wake Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika hawajulikani waliko baada ya kukamatwa na jeshi la polisi siku ya Jumapili.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam mchana wa siku ya Jumatatu Agosti 12, 2024 Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara Benson Kigaila amesema kuwa kukamatwa kwa viongozi hao wakiwemo wanachama wa chama hicho, vijana ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja.
“Polisi watuambie wana malengo gani na Makamu (Tundu Lissu) ambaye wanajua anatumia dawa (kutokana na maumivu ya risasi alizopigwa Dodoma mwaka 2017), wamemkamata, wamemfisha hatujui yuko wapi na hajapewa dawa zozote”
“Polisi mpaka leo hawajaonesha hawa Viongozi wako wapi na hakuna Mwanasheria wala Kiongozi wa Chama ambao tumewatuma kule waliofanikiwa kujua angalau wako wapi”
Kigaila ameongezea kwa kusema “Tunataka tuseme Serikali ya Samia Suluhu Hassan itusikie, Jeshi la Polisi watuelewe, tunataka Viongozi wetu wote waliokamatwa, Wanachama wote waliokamatwa, tunataka waachiwe mara moja bila masharti yoyote, hatutoruhusu na hatutokuwa tayari kuacha Viongozi wetu hawa na Wanachama waliokamatwa bila sababu walale kwenye sero za Polisi leo, wawaachie mara moja bila masharti yoyote”