Mbunge wa Makete na Mwenyekiti wa Bunge Marathon, Mhe. Festo Sanga, ameonyesha mshikamano wa hali ya juu kwa kuungana na Wanajeshi wa Kusambaza Tabasamu (JLKT) katika CRDB Bank Marathon 2024 iliyofanyika nchini Burundi. Mhe. Sanga alishiriki katika mbio hizo kwa lengo la kuchangia misaada kwa wahanga wa mafuriko ya Ziwa Tanganyika, hususani katika mkoa wa Gatumba, Bujumbura.
Mhe. Sanga aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kwa jitihada zao za kupeleka tabasamu nje ya mipaka ya Tanzania. Alisisitiza kuwa hatua hii siyo tu inasaidia wahitaji bali pia inaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano na nchi jirani kama Burundi. Mhe. Sanga aliendelea kusema kuwa jitihada hizi zinaunga mkono sera na mikakati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha mahusiano ya kimataifa na majirani.
Mbio hizi za CRDB Bank Marathon 2024 zimeleta matumaini mapya kwa waathirika wa mafuriko katika mkoa wa Gatumba, na ushiriki wa Mhe. Sanga pamoja na JLKT umekuwa ni ishara ya upendo na mshikamano kutoka Tanzania kwa majirani zao wa Burundi. Wakazi wa Gatumba na washiriki wengine wa mbio hizo walipokea msaada huo kwa shukrani kubwa, wakieleza kuwa tabasamu hilo litaleta faraja kubwa kwao katika kipindi hiki cha changamoto.
Tukio hili limeonyesha jinsi ambavyo ushirikiano wa kikanda unavyoweza kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, na pia umuhimu wa mashirika na taasisi za kifedha kama Benki ya CRDB katika kusaidia jamii zilizo na uhitaji mkubwa.
#KonceptTvUpdates
#CRDB Bank